Simba yajiandaa kisaikolojia, Yanga yatamba kuendeleza burudani
Mtaani raia husema, ‘ni noma sana’ , sasa ni hivi..! Pambano la watani wa jadi nchini Tanzania kati ya Simba na Yanga lazima lipate mshindi.
Bila shaka huzuni na butwaa litawakumba mashabiki wa timu moja kati hizo mbili kongwe za Afrika Mashariki kwani timu moja itatakiwa kushiriki fainali ya Ngao ya Jamii.
Timu hizo kubwa na kongwe zinazobeba taswira ya soka la Tanzania na Afrika Mashariki, zitavaana majira ya saa 1:00 usiku kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam
Pambano lingine nusu fainali litawakutanisha matajiri wa jiji la Dar es Salaam, Azam FC dhidi ya Coastal Union katika dimba la New Amaan Complex kule visiwani Zanzibar.
Kuelekea mchezo huo, mashabiki wa Yanga wanatamba kuwa kikosi chao kiko kwenye kiwango cha juu kikiongezewa nguvu na wachezaji mastaa wanaolijua vyema soka la Bongo, Clatous Chama (Mzambia) , Duke Abuya ( Mkenya) , Prince Dube (Zimbabwe) na Jean Baleke (Mkongomani) hivyo hivyo wanatamba kuendeleza ubabe wao kwa kuifunga Simba kama walivyofanya msimu uliopita, walipoifunga mara mbili kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwemo 5-1 kwenye mchezo wa Ligi.
Kwa upande wa wanachama na mashabiki wa Simba nao wameonekana kuwa na matumaini mapya, hasa baada ya kufanya usajili mkubwa wa wachezaji kutoka Ivory Coast, Zambia, Nigeria, Guinea, Burkina Faso na sehemu mbalimbali.
Wachezaji kama Valentin Nouma Joshua Mutale, Debora Fernandes, Jean Ahoua, Augustine Okejepha, Awesu Awesu, na wengineo wameanza kuwapa kiburi mashabiki wa Simba ambao wamesema wanaweza kupata ushindi, lakini hata kama watapoteza mechi hiyo, haitokuwa kizembe kama walivyochapwa mabao 5-1 msimu uliopita.
No comments